Dk. Gambo: kujinyima chakula wakati wa ujauzito, unyonyeshaji ni kosa kiafya

Dk. Gambo: kujinyima chakula wakati wa ujauzito, unyonyeshaji ni kosa kiafya

Diet ni neno la kingereza lenye maana ya mlo, ingawa jamii yetu imekuwa ikilitafsiri neno hili tofauti.

Wengi wao wanalitafsiri neno diet kama ni kitendo cha kujinyima kula ili kuweza kupunguza uzito, kitu ambacho ni tofauti na wataalamu wasemavyo.

Hivi sasa kumekuwa na tabia ya wanawake wengi wajawazito au wanaonyonyesha kusema kuwa wanafanya diet ya kupunguza kula ili wasiweze kunenepa.

Wakizungumza na Mwananchi kuhusiana na tabia hiyo, watalaam wa afya wanasema hairuhusiwi kwa mjamizto ama anayenyonyesha kujinyima kula.

Mtaalamu wa lishe kutoka Shirika la World Vision, David Gambo anasema njia sahihi ya mlo wa mama mjamzito na anayenyonyesha ni kuzingatia kula mlo kamili wenye virutubisho (Viini lishe) vinavyotokana na makundi yote matano ya vyakula.

Anabainisha makundi hayo kuwa ni wanga (nafaka, mizizi na ndizi mbivu), mimea jamii ya kunde na vyakula vyenye asili ya wanyama, mafuta na sukari, mbogamboga pamoja na matunda.

“Kujinyima chakula (kufanya dieting) wakati wa ujauzito au wakati wa unyonyeshaji ni kosa la kiafya kwani utasababisha mtoto kutopata viinilishe vya kutosha ukuaji wake tangu mimba mpaka utoto wake kwa umri wa miaka 5. 

“Pia madhara ya kujinyima ni kwa mama kudhoofu na kutokuwa na maziwa ya kutosha kwa mtoto hali ambayo itasababisha mtoto kutokushiba vizuri,” anasema Dk Gambo.

Anabainisha kuwa kitendo cha mjamzito au anayenyonyesha kula sana siyo tatizo lakini inategemea mtu huyo anakula chakula cha aina gani hasa kwa kipindi cha miezi sita 6 ya kwanza ambapo anatakiwa ale chakula cha kutosha kwa ajili yake na mtoto.

“Lakini inatakiwa kadri mtoto anavyoongezeka kiumri mama anatakiwa kupungua uzito kwa kupunguza aina ya ukubwa wa milo na aina ya chakula ili kurudi kuwa na uzito wake wa kawaida sawa na uzito alikuwa nao kabla ya ujauzito au kujifungua.

“Hairuhusiwi kuacha kula wanga, mafuta na protini kwasababu ndio makundi makubwa ya chakula na yanayosaidia vitamini na madini kuongezeka. Hakikisha unakula kiasi cha wanga kisichozidi ngumi yako (Wali au ugali au chapati nk) wanga usiokobolewa unashauriwa…pia mafuta yasiwe mengi kwa chakula ila pia ukiwa na uwezo tumia mafuta yatokanayo na mimea kama ya alizeti, ufuta, karanga nk,” anasisitiza.

Hata hivyo anasema inatakiwa kuepuka vyakula vya viwandani vyenye sukari kama vile soda na bia.

“Aepuke vyakula vya kiwandani na vyenye sukari kama soda na bia japo mnaimba bia tamu lakini si bora kwa afya. Pia milo mikubwa iwe asubuhi na mchana ila jioni kwa kuwa mnaenda kulala kula milo laini,” anasisitiza.

Naye Mratibu wa lishe Manispaa ya Temeke, Dk Charles Malale anasema mwili wa mjamzito na anayenyonyesha unahitaji virutubisho vya kutosha ambavyo vinavyofanya kazi katika mwili wa binadamu.

Anasema endapo watajinyima kula hususani vyakula vya wanga na mafutakutasababisha upungufu wa madini pamoja na vitamin.

“Kula chakula kwasababu kila chakula kina umuhimu wake. Kwa mfano ukijinyima vyakula vya mafuta kutasababisha upungufu wa baadhi madini ambayo yatamletea shida katika mwili wake na vitamin

Sio sahihi kwani wanasababisha matatizo kwa mtoto kwasababu wanatakiwa wale ili kuzalisha chakula kwaajili ya mtoto na virutubisho kwaajili ya miili yao, Sasa mtu anayefanya diet anakuwa na changamoto nyingi kwasababu

Lakini huyu mtu anaweza kupungua uzito hata kwa kutokujinyima baadhi ya vyakula isipokuwa anachotakiwa ni kula mlo kamili

Mtu yeyote akila mlo kamili kama ambavyo inapaswa uzito hautoongezeka na atabaki katika hali anayoitaka, lakini sio sahihi mtu kujinyima chakula ili apungue uzito

 Muhimu kula mlo kamili halafu afanye mazoezi

Kunenepa ni moja wapo ya athari zinazotokana na ulaji usiofaa. Kula chakula katika utaratibu usiofaa unaweza kukusababishia kuzidisha lishe au kupunguza lishe 

Kwahiyo lishe inapozidi na unapata huo unene uliokithiri na inapopungua ndo unapata kwashakoo. Lakini ukila mlo kamili huwezi kupata hivyo vitu

Wanasaikolojia wanavyosema

Mhadhiri Msaidizi wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Chama cha Wanasaikolojia (TAPA), Shagembe Magolanga anasema ukuaji wa mtoto unaanzia tumboni ile siku ya kwanza mimba inapotungwa, kile ambacho kinaendelea wakati mama akiwa mjamzito kina mchango wa chanya au hasi katika makuzi ya mtoto

Watoto wanagawanyika katika makundi tofauti, la kwanza ni la mchanga hadi miaka miwili hawa watoto, ahitaji yao makubwa wanategemea sana uangalifu kutoka kwa wazazi au walezi wao ili kupata mahitaji yao ya msingi

Kwahiyo wanapokuwa hawashibi kisaikolojia wanatengeneza kitu kinaitwa kutokujiamini na kuiamini dunia na wakishiba wanatengeneza kujiamini na kuiamini dunia

Kwa maana ya kwamba wale wachanga ambao wazazi wanakidhi mahitaji yao ya msingi, akipata njaa ananyonyeshwa kwa wakati anashiba, akijisaidia anabadilishwa mara kwa mara analazwa mahali ambapo ni salama kwa mtoto

Huyu anakuwa na nafasi nzuri ya kujiamini na kuona kwamba dunia ni sehemu salama, kinyume chake ni tofauti na watoto ambao wazazi hawawajali, hawawanyonyeshi kwa wakati na hawashibi hua wanakuwa hawajiamini na kuona duniani ni kama mahali pa kuteseka

 Na hii hupelekea kupata hasira, muda wote wanakuwa ni watu wa kujishtukia tu, hata mahusiano yao na watu wengine yanakuwa na wasiwasi Ukubwani anakuja kuwa mtu ambaye hulka yake anakuwa ni mtu mgumu kuamini watu wengine na hata akihakikishiwa asilimia 99, yeye atatafuta moja tu ya kutokumuamini

Mwanasaikolojia Barnabas Nkinga, anasema Watoto wadogo hasa umri chini ya miaka miwili huhitaji sana muunganiko wa hisia Kati Yao na wazazi au walezi ambayo kitaalamu huitwa Kwa kiingereza attachment.

Muunganiko huu wa kihisia Kati ya mzazi na mtoto hupatikana pale ambapo mzazi anampatia mtoto mahitaji yake kama chakula, ukaribu wa kimwili, muda wa kutosha kulala na kumsaidia kuwa na kiwango sahihi cha joto mwilini yaani kumuogesha wakati wa joto Kali na kumkumbatia au kumfunika vizuri wakati wa baridi.

Katika kutimiza mahitaji yao mzazi anapaswa kumpatia mtoto mahitaji yake Kwa wakati na kutosheleza. Njia kuu ya mtoto mdogo kutumia kufikisha taarifa ni kupitia kulia Kwa Aina mbalimbali kulingana na hitaji.

Mtoto anaweza kulia kwasababu ya njaa, usingizi, joto au hata kuhitaji uwepo wa karibu wa mzazi. Mzazi asipompatia hitaji husika kwa wakati humpatia mtoto msongo na kujihisi upweke na hajaliwi hivyo kuona kuwa dunia si mahali salama kwa yeye kuishi.

Mtoto asipopatiwa mahitaji yake kwa wakati na kwa kutosheleza mara kwa mara huathiri ukuaji wake kisaikolojia kupelekea kutoamini watu, kukata tamaa wakati wa nyakati ngumu na pengine hata kuwa mwenye hasira.

Hivyo kwa ushahidi wa Saikolojia ni kweli kuwa mtoto kutokushiba inawezasababisha hasira kwa maana hitaji lake la kupata chakula cha kutosha linakuwa halijafikiwa. Kiwango cha hasira itategemea ni mara ngapi hali hiyo inajitokeza.

 

 

 

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags