Msanii wa muziki wa Hiphop nchini Rashid Makwiro maarufu 'Chid Benz', amehoji kuhusiana na baadhi ya wasanii kuimba nyimbo zenye kutaja majina ya wachezaji huku akidai kuwa endapo wachezaji hao wakiondoka nyimbo hizo hazitakuwa na nguvu tena.
Chid ameyasema hayo leo Septemba 10, akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam huku akitolewa mfano wimbo wa Harmonize alioimba kuhusu Yanga 'Yanga Bingwa'
"Nampongeza sana Harmonize nampenda sana kijana mdogo anavyopenda kuhangaika harakati zake za muziki. Mimi ni shabiki wa Yanga toka mdogo wimbo wa Harmonize mzuri sana ule wa Yanga lakini kataja wachezaji kina Aucho, Pacome mimi swali langu wale jamaa tutakuwa nao milele? wataondoka watahamia timu nyingize vipi tutaimba nani sasa?
"Vipi itapokuja timu mpya huo wimbo tutakuwa hatuimbi tena au utaimbwa kama historia? hapana unaweza ukaimba tu Yanga makofi yanapigwa uwanjani na ngoma ikawa, biti kali watu wakaimba kutaja wachezaji ni nzuri lakini sasa hawatakaa milele."amesema
Hata hivyo, mwanamuziki huyo hakuacha kugusia tabia ya baadhi ya waandishi wa habari ambao amedai wanamchonganiha na mkali huyo wa 'Single Again' huku ikiwa ni siku moja tu baada ya baadhi ya vyombo vya habari kuandika kuwa Chid aliuponda wimbo wa Yanga
"Nioneeni huruma bado hadi leo mnaniandika nionekane nimemuongelea vibaya Harmonize nyinyi mnavyoandika mnatafuta watu wasome lakini Harmonize naye anahisia,"amesema
Ikumbukwe kuwa mwaka 2020 Chid alimjia juu Harmonize baada ya kumtaja katika orodha wasanii watakaomsindikiza kwenye tamasha lake la
Jipongeze na Twist Tour' lililofanyika Viwanja vya Mwembe Yanga, Dar es Salaam bila kuwasiliana naye.
Leave a Reply