CCM yatoa maelekezo kumaliza sintofahamu ununuzi wa mahindi Songea

CCM yatoa maelekezo kumaliza sintofahamu ununuzi wa mahindi Songea

 

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimewataka wakala wa chakula NFRA kuweka utaratibu mzuri ili kumaliza sintofahamu iliyopo juu ya ununuzi wa mahindi Manispaa ya Songea kwa kuhakikisha wananchi wote waliokwisha kuorodheshwa Mahindi yao yananunuliwa pamoja na kuongezwa kwa kituo kimoja cha ununuzi wa mahindi ili kuepuka msongamano katika kituo kinachotumika sasa na kuwaondolea wananchi usumbufu.

Hayo yalielezwa na katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka alipotembelea wakala wa Taifa wa chakula (NFRA) na kujionea zoezi la ununuzi linavyoendelea pamoja na kusikiliza wakulima waliokuwa na mahindi nje ya geti la wakala huo.

"Serikali ya CCM inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imekwishatoa shilingi bilioni 7.5 kwa ajili ya ununuzi wa tani elfu kumi na tano katika hatua za awali kwa NFRA hapa Songea Mjini na fedha hizo tayari zipo kwenye akaunti zao, chama kinaitaka NFRA kutoa kipaumbele kwa wananchi wote waliokwisha kuorodheshwa na kuongeza kituo kingine cha ununuzi wa mahindi ili kuepuka huu msongamano na kuwaondolea wananchi wa pembezoni usumbufu." Alisema Shaka

Shaka aliwataka wananchi kuondoa wasiwasi kwani serikali imepanga mgao wa tani elfu thelathini na tano katika msimu huu kwa mkoa wa Ruvuma. Bado serikali inaendelea kutafuta masoko zaidi nje ya Nchi ili kuhakikisha mahindi yote yanapata soko. Aidha aliwaomba wananchi kuwa wakati ununuzi ukiendelea mahindi zaidi yasishushwe hadi yaliyopo yatakaponunuliwa yote ili kuepuka hasara.

Shaka alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Mheshimiwa Dkt Damas Ndumbaro kwa kuwa mtetezi wa kweli wa wananchi anaowawakilisha. Pia aliwapongeza NFRA kwa kujiongeza na kutafuta ghala la ziada litakalotumika kuhifadhi mahindi tani elfu kumi na tano zitakazonunuliwa sasa.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags