Bony Mwaitege asikitishwa kuzushiwa kifo

Bony Mwaitege asikitishwa kuzushiwa kifo

Msanii wa nyimbo za Injili, Bony Mwaitege amesikitishwa na watu ambao wamemzushia kifo katika mtandao wa kijamii.

Mwaitege amezungumza na Mwananchi akisema yeye ni mzima wa afya na amesikitishwa na kushangazwa na uzushi huo wa kifo akibainisha anapigiwa simu nyingi na watu wake wa karibu akiulizwa kuhusu suala hilo.

"Aisee pole sana dada yangu, mimi ni mzima wa afya njema, sijafa. Huu ni uzushi tu wa watu. Kwa kweli nimesikitika sana. Nimeanza kupigiwa simu na watu kutokea Nairobi na Dar na mikoa mingine, hii ni mbaya sana, hapa sasa hivi nipo njiani naelekea Nairobi kwenye kazi za Injili Mungu ni mwema," amesema Mwaitege.

Mwananachi ilimuuliza pia kuhusu madai kwamba ametengeneza kiki akidaiwa ana kanisa lake, akasema sio kiki kwani kwa hatua aliyopo yeye si mtu wa kuhitaji kufanya kiki anapofanya jambo lake.

"Kwanini nifanye kiki? Yaani kiki ndio nijiue mwenyewe? Kwa hatua niliyofikia ya kazi ya sanaa yangu sio ya kufanya kiki ndio nifanye kitu," amesema Bony.

Kwa upande wa mwanamuziki wa nyimbo za Injili, Flora Mbasha, amezungumza na Mwananchi kuhusu uzushi huo wa kifo cha Bony Mwaitege akisema alizisikia taarifa hizo na kwamba ziliwaathiri watu wengi.

"Hizi habari mimi niliziona tu kwenye mitandao, ni habari ambazo sio nzuri kabisa, kuna baadhi ya watu wanamzushia kifo mtu kwa maslahi yao tu. Hii habari ya Bonny Mwaitege imewaathiri watu wengi sana kitu ambacho sio kizuri," amesema Flora.

Bony Mwaitege ametamba na nyimbo nyingi zikiwemo kama 'Safari Bado', 'Dunia Dunia', 'Acha Nizaliwe', 'Bado Nampenda' na 'Mke Mwema' ambao zimempatia umaarufu mkubwa.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags