Bongo Movie ilivyowapa kisogo mamisi

Bongo Movie ilivyowapa kisogo mamisi

Tangu kuanzishwa kwa mashindano ya kusaka warembo,  Miss Tanzania mwaka 1967 tayari imepita miaka 57,  huku taji hilo likiwa limevaliwa na warembo 30 hadi kufikia mwaka 2023, ambapo lilichukuliwa na Tracy Nabukeera.

Kinachosababisha utofauti wa miaka ya mashindano hilo na idadi ya warembo walionyakua taji, ni kutokana na baadhi ya miaka shindano hilo kutofanyika.

Licha ya kuwa uanzishwaji wa mashindano hayo ya kusaka walimbwende miaka ya nyumba kuonekana yakizalisha waigizaji wa Bongo Movie, kwa sasa jambo hilo limekuwa tofauti kwani waongozaji filamu wamejikita zaidi kuibua vipaji vipya kutoka mtaani na si kuchukua warembo wa shindano hilo kama ilivyokuwa awali.

Waigizaji waliopita Miss Tanzania

Wema Sepetu

                        

Wema Sepetu alishiriki shindano la Miss Tanzania 2006 na kuondoka na taji hilo, kisha baadaye akaingia kwenye Bongo Movie ambayo alihusika kwenye movie nyingi baadhi zikiwa Family Tears na Red Valentine.

Lulu Diva

Lulu Abbas ‘Lulu Diva’ alishiriki Miss Pwani 2013 na kuwa mshindi wa pili. Kisha akawa mshindi wa Miss Kibaha wa mwaka huohuo. Baada ya hapo akawa kwenye listi ya kushiriki Miss Tanzania hakufanikiwa kushinda.

                       

Baadaye Lulu Diva akaibukia katika muziki wa Bongo Fleva na kufunika na ngoma zake kali kama Usimwache, Homa, Utamu, Nilegeze, ‘Ona’ ft Rich Mavoko, ‘Milele’ ft Barnaba.

Huku akiendelea kubamba katika gemu ya Bongo Fleva, Lulu Diva amejitosa katika fani ya maigizo akitisha katika tamthilia ya ‘Rebecca’ na ‘Jua Kali’ inayorushwa na DStv.

Hamisa Mobeto

                       

Mwaka 2011 Hamisa, alishiriki mashindano ya Miss Dar Indian Ocean na alifanikiwa kushika nafasi ya pili. Mwaka huohuo pia akawa mshindi wa pili wa Miss Kinondoni na kufanikiwa kuingia kwenye nusu fainali ya Miss Tanzania. Mwaka 2012, Hamisa alishiriki kwenye mashindano ya Miss University Afrika na kuingia hatua ya 10 bora. Baada ya kutoka kapa alitumbukia kwenye Bongo Movie.

Irene Uwoya

Ni miongoni mwa nyota wa Bongo Movie waliopitia kwenye Shindano la Miss Tanzania akitokea Wilaya ya Kinondoni mwaka 2006. Uwoya aliibuka kwenye tano bora, lakini baada ya hapo aliangalia upande wa filamu akakubalika, hadi leo anawika na ana jina kubwa nchini.

Uwoya, mbali na kutamba katika filamu za Bongo kwa muda mrefu pia amekuwa akifunika katika tamthilia mbalimbali za televisheni.

Aunty Ezekiel

                        

Alikuwa ni mmoja wa washiriki wa Miss Tanzania 2006, lakini hakuweza kufanya vizuri. Aliamua kuangalia upande mwingine wa uigizaji ambapo kwa mara ya kwanza alionekana kwenye Filamu ya ‘Miss Bongo’. Kuanzia hapo alianza kuwika na mpaka leo hii ni staa mkubwa nchini.

Flora Mvungi

Flora Mvungi aliwahi kuwa Miss Pwani 2008, alinyakua taji la Miss Kanda ya Mashariki kwa mwaka huo. Aliposhindwa katika shindano la taifa la Miss Tanzania, akageukia kwenye fani ya kuigiza na hadi sasa ana jina kubwa hapa nchini.

Jokate Mwegelo

Alishiriki shindano la Miss Tanzania mwaka 2006 na kukamata nafasi ya pili. Baada ya kushindwa kutwaa taji hilo aliendelea kufanya mambo mengine ikiwamo ujasiriamali kupitia brandi yake ya Kidoti na pia kujiingiza kwenye uigizaji wa filamu.

Mwaka wa 2007, alipata kucheza filamu yake ya kwanza iliyojulikana kwa jina la Fake Pastors, akiwa na Vincent Kigosi, Lisa Jensen, mshindi wa tatu wa Miss Tanzania 2006 na marehemu Adam Kuambiana. Mwaka wa 2008, alicheza katika filamu ya ‘From China With True Love’.

Mwaka wa 2010, alionekana katika filamu ya ‘Chumo,’ filamu iliyoandaliwa na Media for Development International, kuhusu elimu juu ya ugonjwa wa malaria. Filamu hii ilimwezesha kupata tuzo ya Zanzibar International Film Festival (ZIFF) akiwa kama mwigizaji bora wa kike kwa 2011.

Jokate aliyezaliwa Machi 20, 1987, mbali na uigizaji wa filamu, pia ni mjasiriamali na mwanasiasa.

Chuchu Hans

Naye alianzia kwenye Shindano la Miss Tanzania mwaka 2005, akitokea jijini Tanga. Chuchu aliibuka kidedea kwenye Miss Talent. Baada ya hapo alijitumbukiza kwenye filamu na mpaka sasa ni mwigizaji mzuri. Alianza kutamba kwenye filamu yake ya kwanza ya ‘Roho Sita’.

Baby mama huyu wa muigizaji Vincent Kigosi, aliyezaa naye mtoto mmoja, kwa miaka mingi sasa amekuwa akitisha katika anga la filamu na tamthilia nchini.

Miriam Jolwa ‘Jini Kabula’

Alishikilia Taji la Miss Kariakoo miaka ya nyuma lakini alishindwa kutwaa taji la Miss Tanzania. Baadaye akageukia kuigiza na alianza kuwika kwenye tamthilia ya luninga ya ‘Jumba la Dhahabu’ iliyompa jina la Jini Kabula.

Sababu waongozaji filamu kutotumia ma-miss

Akizungumza na Mwananchi mwongozaji filamu nchini Neema Ndepanya amesema kuwa soko la zamani lilikuwa linahitaji zaidi watu maarufu lakini kwa sasa hali ipo tofauti.

“Mitaani kuna vipaji vingi na vikubwa sana ambavyo mwanzoni tulikuwa hatuvipi nafasi sababu soko la zamani lilikuwa linahitaji sana watu wanaojulikana ikiaminika kuwa ndiyo wanaouza zaidi.

“Sasa mambo yamebadilika na hata watazamaji wamekuwa na mitazamo tofauti siyo kama ya zamani, wanaangalia zaidi nani anatendea haki nafasi anayopewa na wenye vipaji wanapokelewa vizuri,”anasema.

Kwa upande wa Abdul Juma, ambaye pia mwongozaji wa filamu mbalimbali nchini amesema walikuwa wanatumika zaidi warembo hao kwa sababu ya majina yao kwani upepo wa kipindi hicho ndivyo ulivyokuwa unataka.

“Nadhani ni upepo enzi hizo, lakini kwa sasa tunajaribu kukua zaidi hapo mwanzoni ilikuwa inafanyika hivyo lakini haikuwa mbaya kwa sababu hata hao mabinti bado walivaa viatu vya uigizaji vizuri na kuipa heshima tasnia,” alisema.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags