Mfanyabiashara wa madini na bilionea nchini Australia, Gina Rinehart, ameliomba jumba la Sanaa la Kitaifa la ‘Canberra’ nchini humo kuondoa picha yake ambayo hajapendezwa nayo.
Kwa mujibu wa gazeti la ‘The Sydney Morning Herald’, Rinehart alipeleka ombi hilo kwa Mkurugenzi wa jumba hilo Nick Mitzevich na Mwenyekiti wa Ryan Stokes Aprili mwaka huu kuhusu kuondolewa kwa picha hiyo.
Licha ya ushawishi wake mkubwa na kutajwa kumiliki zaidi ya dola bilioni 30 lakini jumba hilo la Sanaa limekataa kufuata matakwa ya kuondoa picha hiyo kwa lengo la kudumisha haki ya msanii aliyechora.
Picha hiyo ilitambulishwa rasmi na picha nyingine ishirini katika maonesho ya ‘Australia in Colour’ siku chache zilizopita ikiwa imechorwa na msanii maarufu Vincent Namtjira.
Ingawa Gina Rinehart, bado hajaingia kwenye orodha ya wanawake matajiri zaidi duniani kwa sasa, lakini Forbes inaonesha kuwa mwanamama huyo anamiliki utajiri wa dola bilioni 30.2 kwa mwaka 2024.
Leave a Reply