Biashara ya saa, mabegi, ilivyobadilisha maisha ya Swabri

Biashara ya saa, mabegi, ilivyobadilisha maisha ya Swabri

Kama tulivyokubaliana katika makala zetu za nyuma kuwa katika upande wa biashara sasa tumeamua kuwasogeza vijana na wachakarikaji ambao wanaendesha maisha yao kupitia biashara mbalimbali wanazofanya.

Licha ya kuwepo na vikwazo vingi katika baishara ya kuuza vifaa mbalimbali vya simu lakini biashara hiyo imemuondoa Mohamed Swabri katika dimbwi la umaskini na kumfanya aweze kumiliki duka la saa, vifaa vya simu na mabegi.

Swabri alifunguka kupitia Mwananchi Scoop jinsi alivyoanza biashara hiyo kwa kuwauzia wanafunzi alipokuwa akisoma mpaka kufungua duka ambalo ndiyo chanzo chake cha kipato na kinachoendesha maisha yake kila siku.

“Kwanza kabisa mimi napenda kufanya biashara, jambo jingine ambalo limenisukuma kuamua kujiajiri ni kutokana na ugumu wa maisha pamoja na umasikini, ukiachilia mbali hayo yote niliwahi kuajiriwa kama kibarua lakini hakuna pesa ya maana ambayo nilikuwa naipata ndipo nikapata wazo la kufanya biashara ambayo watu wengi wamekuwa wakiichukulia poa” amesema Swabri

Siku zote waswahili wanasema biashara ni kama kamari, kuna kupata na kukosa kwa upande wa kijana huyo amefunguka kuhusiana na faida anazopata kupitia biashara hiyo

“Kwa hapa nilipofikia nimepata faida kubwa sana kwanza kabisa nimekuwa ni mtu ambaye naaminika, brand yangu inakuwa kila kukicha hadi kwenye mauzo yameongezeka, kwa sasa faida kubwa niliyoipata ambayo inanifanya niiheshimu hii biashara ni kunifanikisha kununua kiwanja na kuanza kujenga” amesema Swabri

Aidha kijana huyo aliongezea kwa kueleza kuwa ili uweze kuwa mfanyabiashara ambaye unahitaji kuyaona matunda ya biashara yako unatakiwa kuwa na malengo na kuiheshimu biashara huku akimtaja mfanyabiashara Niffer ambaye amefungua Mall hivi karibuni kama mfano wa wafanyabiashara ambao wanaheshimu na kuzithamini biashara zao.

Ushauri kwa vijana
“Ushauri wangu kwa vijana kwanza maisha ni magumu so kama kijana kuna umuhimu wa kujitambua kwa mambo haya, kwanza kujua wewe ni nani katika familia na jamii, pili unataka nini au kuwa nani katika maisha yako, tatu hatua gani umechukuwa kufanikisha unachotaka au kuwa nani jiamini jikubali na kujituma kila kitu kinawezekana kwa uwezo wa Mungu” amesema

Role Model wake
Vijana wengi hufuata nyayo za wanasiasa na wanamitindo mbalimbali lakini kwa Mohamed Swabri kwake ni tofauti ameweka wazi kuwa yeye ‘Role Model’ wake ni mfanyabiashara mkubwa ndani na nje ya Tanzania Said Salim Bakhresa.

Swabri ameeleza kuwa anatamani kuwa kama Bakhresa kwa sababu ya ubunifu wake na uthubutu katika biashara, huku ndoto yake kubwa ikiwa kufanya biashara kwa bidii kwa ajili ya kubadilisha maisha yake na ya familia yake kwa ujumla.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post