Baada ya miaka minne ya mafanikio ya kiuongozi akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu ametangaza kustaafu ifikapo Agosti 31, 2024.
Machumu ambaye amehudumu kwa muda mrefu katika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya kampuni hiyo hadi kufika ngazi ya mkurugenzi mtendaji, ametangaza hilo leo Jumatatu Juni 3, 2024 katika kikao cha wafanyakazi kilichofanyika makao makuu ya kampuni, Tabata Relini, Dar es Salaam.
Kustaafu kwake ni sehemu ya mkakati wake wa muda mrefu wa mabadiliko ya uongozi, ili kuhakikisha kuna mwendelezo wa safari aliyoianza kama kinara wa mageuzi, aliyeongoza MCL kutanua wigo wake kibiashara, kutoka uchapishaji magazeti hadi kuwa mtandao mkubwa zaidi wa habari na huduma kidijitali Tanzania.
Akizungumza katika kikao cha wafanyakazi leo, Mwenyekiti wa Bodi ya MCL, Leonard Mususa amemtangaza Victor Mushi, ambaye kwa sasa ni Mhariri Mtendaji Mkuu, kukaimu nafasi hiyo wakati Bodi ya MCL ikiendelea na mchakato wa kutafuta mkurugenzi mtendaji mpya.
Machumu alijiunga na MCL Julai 2004 kama Mhariri wa Biashara wa gazeti la The Citizen. Kuanzia Mei 2006 hadi Desemba 2013, alishika hatamu ya The Citizen kama Mhariri Mtendaji, akiiongoza kujipambanua kama chombo bora zaidi cha habari za biashara nchini Tanzania.
Desemba 2013 hadi Julai 2020, alipewa jukumu la kuongoza divisheni ya habari kama Mhariri Mtendaji Mkuu. Katika nafasi hiyo, aliwezesha mageuzi jumuishi ya biashara ya habari wakati wa mapinduzi makubwa ya kidijitali ya tovuti, akiiongoza MCL kutoka kuendeshwa kwa nadharia za uhariri, hadi kuongozwa na taarifa, maarifa na matakwa ya hadhira, huku uhabarishaji ukizingatia misingi bora ya ubunifu wa kidijitali na kuyapa kipaumbele mahitaji ya wasomaji.
Leave a Reply