Pallazo pants (bwanga) ni moja kati ya mtindo wa suruali ambao umedumu kwa muda mrefu katika tasnia ya mitindo.
Kama ilivyo katika mitindo mingi ya mavazi inayoibuka, pallazo pants nayo huibuka na kupata mashiko kisha hutoweka na baada ya muda fulani hurudi tena.
Mtindo huo huweza kuwa katika mfumo wa aina mbalimbali za vitambaa, vitenge, batiki, vikoi na nyinginezo.
Inaelezwa kuwa mtindo huu ulianza kuvaliwa katika kipindi cha miaka ya 1920 -40 na kuwahi kuvaliwa na baadhi ya wanawake maarufu na wenye ushawishi kama vile Katharine Hepburn, Greta Garbo and Marlene Dietrich.
Ilipofika miaka ya 1960-70 mtindo huo ulizidi kupata umaarufu na kuanza kuvaliwa kwa wingi kwa mujibu wa tovuti mbalimbali za masuala ya mitindo.
Wabunifu nao wamekuwa wakitumia taaluma na vipaji vyao katika kuweka ubunifu katika mtindo huu na kuufanya uonekane kama mpya kila unapoibuka.
Hadi sasa aina hiyo ya suruali imeendelea kujizolea umaarufu na kuvaliwa na watu mbalimbali haswa wanawake.
Amina Abdallah, mkazi wa Chanika, jijini Dar es Salaam anasema bwanga ni moja kati ya nguo ambayo huifurahia zaidi anapoivaa kwa kuwa haibani hivyo inamfanya kuwa huru kufanya shughuli zake.
“Katika msimu wa joto huwa sipendelei kuvaa nguo zinazonibana sana hivyo bwanga huwa ni mkombozi wangu,”anaeleza.
Akizungumza na Mwananchi Scoop muuzaji wa nguo na viatu vya kike kutoka Hobby Fashion, Shania Shabani anasema kuwa bwanga ni aina mojawapo ya suruali ambayo hupendwa haswa na wanawake.
Anasema moja ya sababu inayowapelekea baadhi ya wanawake kupendelea kuvaa aina hiyo ya suruali ni namna inavyowaweka huru kutembea, kuruka na hata kucheza kutokana na kuwa pana.
“Pia bwanga humpendeza mtu mwenye mwili wa aina yeyote, cha msingi ni kuzingatia upana na namna ya kuipangilia kulingana na mwili wa muhusika. Ni mtindo wa suruali usio na mambo mengi na hudumu kwa muda mrefu kwani baadhi ya aina ya mabwanga huweza kuvaliwa hata mtu anapoongezeka mwili kidogo,” anasema.
Shani anaeleza kuwa mtindo huo wa suruali unapendeza kuvaliwa na shati, ‘tshirt’, blauzi ya mikono mirefu, mifupi aina ya off- sholder au iliyofunika shingo.
“Vilevile bwanga huweza kuvaliwa na bodysuit, turtle necks ya mikono mirefu au mifupi, blazer, au croptop jambo la msingi kuzingatia kabla ya kuchagua aina gani ya nguo kuvalia bwanga lako ni kuzingatia muda, majira na mahala unapokwenda,” anasema.
Akatolea mfano kipindi cha baridi kali haishauriwi kuvalia bwanga blauzi isiyo na mkono kwani itapelekea baridi kufikia maeneo yaliyo wazi na nyakati za joto kali haishauriwi kuvalia turtle necks ya mikono mirefu kwani inaweza kupelekea aliyevaa kuhisi joto zaidi.
“Ni muhimu pia unapovaa mtindo huu kuzingatia uwiano wa rangi kati ya nguo ya juu na bwanga, kama bwanga lina rangi nyingi au michoro mingi inapendeza nguo itakayovaliwa juu kuwa ya rangi moja.”
Alieleza kuwa mtindo huo unaweza kuvaliwa katika shughuli mbalimbali ikiwemo zile zinazohusiana na michezo, burudani, mitoko ya ufukweni na nyinginezo kulingana na namna utakavyoipangilia.
Ebwanaaa eeeh bila shaka wiki hii utakua umenipata vyema kabisa kwenye anga za fashion unaweza kutoa maoni yako wiki ijayo ungependa tugusie mtindo upi wa nguo? Nakutakia siku njema.
Leave a Reply