Vipo vitu vingi ambavyo vimekuwa vikitumia kwenye jamii na kuleta manufaa bila ya watumiaji kufahamu ni nani aliumiza kichwa kubuni vitu hivyo.
Kutokana na hilo mfahamu raia wa Marekani William Phelps Eno ambaye ndiye mvumbuzi wa kwanza wa alama za usalama wa barabarani.
William ambaye wengi walimfahamu kwa jina la ‘Baba wa Usalama wa Barabarani’, mwaka 1867, akiwa barabarani alikumbana na msongamano wa magari ya farasi, ndipo alipopata wazo la kubuni alama hizo.
Mwaka 1900, Eno aliandika makala kwenye Gazeti la The Rider and Driver kuhusu msongamano, jambo lililosababisha kuundwa kwa sheria za kwanza za barabarani za New York.
Baadhi ya mawazo aliyopendekeza katika makala hiyo ni ishara za kubadilisha njia, ishara za kupunguza kasi na kusimama na wazo kwamba magari yanapaswa kubaki kwenye upande mmoja wa barabara (upande wa kulia nchini Marekani).
Alianza ubunifu wake katika barabara zilizokuwa katika ya miji mikubwa kama vile New York, London, na Paris.
Ambapo kati ya alama alizobuni ni sehemu za kusimama teksi, vivuko vya waenda kwa miguu, alama za kusimama, na alama nyinginezo.
Jambo ambalo limekuwa likiwashangaza wengi ni kwamba licha ya kuwa aliyebuni alama za barabarani lakini kwenye maisha yake yote hakuwahi kuendesha gari wala kujifunza badala yake alikuwa akitumia usafiri wa farasi. William alizaliwa 1858 mwaka na alifariki 1945.
Leave a Reply