Penzi la mchepuko likanilevya, nikakinukisha vibaya..!

Penzi La Mchepuko Likanilevya, Nikakinukisha Vibaya..!

Nilikuwa nina kama miezi mitatu tangu kuoa kwangu. Ilikuwani Juni 1995. Mke wangu alikuwa akiniamini sana na hata wazazi wake, hasa mama yake, kwani alinifundisha shule ya msingi, wakati akiwa mwalimu. Mwaka huo wa 1995 alishastaafu.

Siku hiyo nilikuwa nyumbani na mke wangu alikuwa ameenda kwao. Ilikuwa ni mapema bado, kama saa nane mchana, kwa hiyo sikutegemea angerudi wakati ule kwani tulikubaliana kwamba, angerudi jioni.

Nilikuwa nimekaa sebuleni nikiangalia TV. Mara simu yangu ikaita. Nilipunguza sauti ya TV hadi ziro na kupokea simu. Ilikuwa inatoka kwa msichana ambaye nilikuwa nimeanza uhusiano naye kama mwezi mmoja nyuma. Ukweli hadi leo najiuliza niliweza vipi kufanya jambo kama lile, kwani sikuwa kabisa napenda wanawake na nilikuwa pia naheshimu ndoa yangu.

Nilipokea simu na kuanza kuzungumza naye. “Usijali mpenzi kesho nitakuona….. Nani, First Lady? Hana neno huyu na wala hawezi kunishtukia, kwani ananizimikia sana. Nimemshika kwa kweli. Unajua nini, ulichelewa kidogo tu kujitokeza kwangu, lakini pale madhabahuni miezi mitatu iliyopita ungetakiwa kusimama wewe, siyo yeye……” Niliendelea kubwabwanya mwanaume na maneno yalikuwa yananitoka kama muimba taarabu wa mipasho.

“Lakini hata hivyo halijaharibika neno. Huku nimefungwa pingu za kanisani, lakini moyo wangu uko kwako mpenzi. Nakuhakikishia kwamba, nikiwa nawe, kila kitu kinabadilika, kinakuwa supa kwani wewe ndiwe kidundisha moyo wangu. Naanza kumchoka wife ujue, kwani  hata nikiwa naye naiona sura yako kwake…………”

Wakati nikiendelea kumshushia mistari huyo mpenzi wangu mara ghafla nikahisi nywele zimenisimama kisogoni ikabidi ninyamaze na kugeuka nyuma. Nilishtuka kwa njia ambayo ingeweza hata kuniuwa kwa shinikizo.

Nilimwona mke wangu na mama yake wakiwa wamesimama. Nilijifaragua kutaka kuwakaribisha lakini walivyokuwa wananitazama, mwenyewe nilinywea, sauti ikakauka.

“Ulikuwa naongea na nani?” mke wangu aliniuliza .

Nilibabaika kabla sijajibu……. “Ni …….ni… kuna jamaa yangu mmoja….” Sikumaliza kwani niliwashwa kibao cha maana shavuni na mke wangu.

Halafu alinivaa na kunitupa chini. Nilikuwa sina nguvu kabisa, nilikuwa bwege hasa. Kweli kufumaniwa ni kubaya.

Mama mkwe aliingilia kati kwa kuamua kumwondoa mwanaye. Wapangaji upande wa pili wa nyumba nao walifika na kutuamulia .

Mama mkwe alimshika mkono bintiye na kumwambia, “twende, acha kila kitu humu ndani, usichukue chochote. Inatosha kwa haya tuliyoyaona.” Waliondoka na bintiye wakiniacha pale chini nikiji zoa zoa na kusimama huku nikipepesuka.

Wapangaji wa wenzangu wanaoishi nyumba iliyoko upande wa pili walicheka kwa pamoja kicheko cha kebehi  na kumalizia na neno, halo halooooo…..

Walionekana wazi kufurahia dhahama ile, kwani tulikuwa tukiwasema sana kwamba ndoa zao ni za kuunga kwa gundi.

Najua mnataka kujua ilikuwaje baada ya pale.

Acheni umbea, fanyeni kazi……

Lakini ngoja nikate kiu yenu ya umbea. Ni kwamba, baada ya pale, tuliyamaliza na mke wangu na alinisamehe baada ya kumweleza ukweli wote.

Kusema kweli tangu siku hiyo nimebadilika sana. Nikiona mwanamke nisiyemjua ananichekea chekea na kujipendekeza kwangu…….. nafunga viatu vizuri na kutimua mbio…………

 

 
Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Saphinia Suleiman

A writer, reporter, presenter and news anchor for Mwananchi Scoop. Her writings are based on Career and skills development every Monday and entertainment, every Friday on Mwananchi Scoop. Her famous segments on Mwananchi Scoop include SMARTPHONE and NIPE DILI.

Latest Post