Nikapigwa ‘repatriation’ kurudishwa kijijini kwa tuhuma za umbea….

Nikapigwa ‘repatriation’ Kurudishwa Kijijini Kwa Tuhuma Za Umbea….

Nakumbuka ilikuwa ni mwaka 1991 ndipo nilipokutana na  mkasa huu ulionivurugia future yangu ya kusoma.

Ilikuwa ni mwaka huo wa 1991 kaka yangu binamu alinichukua kutoka kijijini kwenda naye Arusha alipokuwa akifanya kazi wakati huo ili kuniendeleza na elimu katika chuo cha ufundi baada ya kutofaulu kuendelea na masomo ya kidato cha tano.

Nilijiona ni mwenye bahati baada ya kusota kijijini kwa mwaka mmoja tangu nimalize kidato cha nne mwaka 1990 na kuangukia pua na hivyo kubaki nikichunga mifugo kijijini huko wilayani Same.

Nakumbuka kulitokea msiba wa mjomba wetu mkubwa ambaye ni baba mkubwa wa huyo kaka yangu binamu na alipokuja kwenye mazishi alivutiwa sana na tabia zangu hasa kutokana na kufanya kazi sana siku ya msiba na nidhamu niliyo kuwa nayo.

Aliongea na baba yangu ambaye ni mjombake ili kujua mustakabali wa Maisha yangu baada ya kumaliza masomo yangu ya sekondari. Kwa bahati mbaya baba wakati huo alikuwa ameachishwa kazi huko wilayani alipokuwa akifanya kazi akawa yuko kijijini akilima ili kujikimu na familia kwa hiyo hakuwa na uwezo wa kuniendeleza kielimu.

Baada ya Baba kumweleza kaka yangu binamu kuhusu hali yake kiuchumi, kaka yangu binamu alimuomba baba anichukue niende naye Arusha alipokuwa anafanya kazi ili akanisomeshe chuo cha ufundi na Baba aliridhia bila kinyongo na alimshukuru sana huyo kaka yangu binamu kwa uamuzi wake wa kunisaidia kunisomesha.

Ni kweli baada ya shughuli za msiba kwisha niliondoka  na kaka yangu kwenda Arusha kuanza Maisha mapya ambapo sasa nilikuwa na matumaini ya kusoma chuo angalau niwe na ujuzi.

Nilipofika Nilikutana na shemeji yangu na wanae wawili wote wa kiume ambao walikuwa bado wanasoma shule ya msingi. Mmoja akiwa darasa la kwanza na mwingine akiwa darasa la pili. Kwa kuwa ilikuwa ni mwezi wa sita kaka alinitaka nisubiri mpaka mwakani ndipo ataniandikisha katika chuo cha ufundi pale jijini Arusha kwa ajili ya kusomea ufundi umeme kama mwenyewe alivyopendekeza.

Kaka yangu na mkewe ambaye ni shemeji yangu wote walikuwa ni watumishi serikalini na kwa bahati mbaya nilipofika hapo nyumbani kwake nilikuta msichana wa kazi amerudishwa kwao baada ya kupata ujauzito.

Kutokana na changamoto hiyo, shemeji yangu alikuwa anaamka alfajiri kuwaandaa Watoto na kuandaa chai na baada ya kunywa chai wanaondoka na kaka lakini yeye anawapeleka Watoto shuleni kwanza ndipo aende kazini kwake. Na hata jioni akitoka alikuwa anawapitia Watoto shuleni na kurudi nao nyumbani.

Baada ya kukuta hiyo changamoto nilianza sasa kuamka alfajiri kumsaidia kazi na akishawaandaa Watoto nawapeleka shuleni ambapo palikuwa siyo mbali sana kisha narudi nyumbani kuendelea na kazi ndogo ndogo ikiwa ni Pamoja na kufua na kupika chakula cha mchana kwa ajili ya Watoto wakirudi shule.

Kutokana na umahiri wangu wa kufanya kazi za nyumbani ikiwa ni Pamoja na usafi na kupika, shemeji yangu alitokea kunipenda sana. Aliniona kama mkombozi wake.

Hata hivyo aliendelea kutafuta mfanyakazi wa Ndani  kwa sababu alikuwa anajua kwamba mwakani nitaanza masomo yangu ya ufundi.

Nakumbuka hata manunuzi ya vyakula vya nyumbani alikuwa ananituma na alikuwa ananiamini kwa sababu nilikuwa ni muaminifu sana. Kaka yangu pia alifurahia sana uwepo wangu pale kwake kwa sababu nilikuwa nasaidia sana kazi ndogo ndogo ambazo alikuwa anatoa fedha kwa vijana wa pale mtaani kuzifanya, kama vile kufyeka nyasi nk.

Siku moja nakumbuka ilikuwa ni siku ya Ijumaa kaka yangu ambaye wakati huo tulishazoeana sana alinituma niende stand ya basi kumpokea mgeni wake ambaye alikuwa ni mwanamke anayetokea Moshi. Alinionyesha picha yake na kunitajia jina la basi alilokuwa anakuja nalo.

Alinipa kiasi cha fedha na kunitaka niende na huyo mwanamke hadi hoteli fulani na kumchukulia chumba na kisha nirudi nyumbani lakini alinikanya nisimwambie shemeji yangu akirudi jioni kwani siku hiyo kaka alirudi nyumbani mapema kabla ya shemeji.

Nilichukua zile fedha na kuelekea stendi ya basi. Lile basi lilipofika nilisubiri abiria washuke. Nilikaa usawa wa mlango wa lile basi mara nikamuona yule mwanamke anashuka, nami bila kupoteza muda nikamfuata na kujitambulisha kwake.

Alikuwa ni mwanamke mrembo kwa sura na umbo ambapo uzuri wake ulinogeshwa na ule weupe wake wa kuzaliwa.

Nilimueleza kwamba nampeleka Hotelini na nitamuacha hapo na kaka atakuja kumuona baadaye. Kwa kuwa hoteli yenyewe ilikuwa mbali kidogo nilichukua taxi kama kaka alivyonielekeza na kuelekea kule ilipo ile Hoteli.

Tulipofika hotelini nililipia chumba na kumkabidhi yule mwanamke funguo na kuondoka lakini safari hii nilipanda basi la abiria maarufu kama vifodi pale Arusha na kurudi nyumbani kutoa taarifa kwa kaka kwamba kazi yake nimeshaifanya na kuikamilisha.

Niliendelea na kazi yangu ya kupiga pasi nguo za familia wakati kaka akiwa anajiandaa kutoka. Hata hivyo kabla hajatoka shemeji akawa amerudi na baada ya kusalimiana kaka akamuaga kwamba anaenda kazini kwake kwani ameitwa na bosi wake mara moja. Shemeji alimuitikia tu na kaka akaondoka.

Baada ya muda mfupi shemeji naye akajiandaa haraka haraka na kutoka lakini hakuaga anakwenda wapi jambo ambalo haikuwa kawaida yake.

Baada ya kama nusu saa shemeji alirudi akiwa anatweta huku akiwa anatokwa na damu kwenye majeraha usoni na mikononi. Alikuwa amefura kwa hasira na alipoingia Ndani alikwenda chumbani kwake moja kwa moja na kujifungia. Nilimsikia akiwa analia huko chumbani.

Ni bahati tu Watoto walikuwa kwa dada yake shemeji anayeishi mtaa wa tatu kutoka pale tunapoishi wakiwa wameenda kucheza na Watoto wenzao na pale nyumbani nilibaki peke yangu.

Nikiwa bado ninajiuliza maswali bila majibu kuhusu kilichompata shemeji mpaka kuwa katika hali ile, ghafla alitoka na begi lake la nguo na kuondoka zake bila kunisemesha wala kuniaga.

Baada ya muda mfupi kaka alirudi akiwa katika hali ile ya kutweta kama vile katoka kupigana na hata shati alilovaa lilikuwa limechanika ubavuni.

Aliponiuliza kuhusu mkewe alipo nilimweleza kwamba shemeji alirudi akiwa analia na amechukua begi la nguo na kuondoka zake.

Kaka alibadilisha nguo haraka na kutoka bila kuniambia anakwenda wapi.

Nilibaki peke yangu pale nyumbani nikiwa sijui ni kitu gani hasa kimetokea.

Ilipofika majira ya saa nne usiku hivi kaka alirudi akiwa amefura kwa hasira na kuanza kunifokea kwamba kwa nini nataka kuvunja ndoa yake. Alilalamika kwamba kujitolea kwake kunichukua ili kunisomeasha ndiyo nataka kumvunjia ndoa yake..

Itaendelea wiki ijayo…..

 


Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Janeth Jovin

A writer, reporter, presenter and news anchor for Mwananchi Scoop. Her writings are based on business, money management on Tuesday and health on Thursday on Mwananchi Scoop. Her famous segments on Mwananchi Scoop include KARIA and FASHION.


Latest Post