Hii ya Mbosso ni Pawa haswaaa

Hii ya Mbosso ni Pawa haswaaa

Peter Akaro

Umetia mwezi mmoja tangu Mbosso, staa wa Bongofleva kutokea Khan Music kuachia Extended Playlist (EP) yake ya pili, Room Number 3 (2025) ambayo imebeba wimbo 'Pawa' unaopendwa na mashabiki wengi.

Kama lilivyo jina lake, yaani Pawa, wimbo huo umekuwa na nguvu zaidi kati ya zile saba zilizojumuishwa katika mradi huo, na sasa Mbosso yupo katika kilele cha mauzo katika majukwaa mengi na makubwa ya kuuza muziki duniani.

Huu ni wimbo wa mapenzi wenye kusisimua unaoelezea nguvu kubwa ya hisia za upendo wa dhati kwa sauti laini, Mbosso anaufananisha upendo na nguvu ya kulevya inayomwacha dhaifu na mwenye msisimko wa kihisia, yaani kuishiwa Pawa.

Maneno ya wimbo yamechanganya udhaifu wa kihisia na heshima ya dhati huku Mbosso akimchora mpenzi wake katika picha kubwa na safi kama chanzo cha nguvu na msukumo wa kweli wa maisha.

Kwa ujumla wake, kupitia mchanganyiko wa midundo ya Bongoflava na ala za muziki wa hisia, wimbo 'Pawa' umeonyesha uwezo wa Mbosso katika uandishi wa mashairi na uimbaji wenye hisia kali za mapenzi.

EP, Room Number 3 (2025) ilitoka rasmi Juni 13, ikiwa ni takribani miezi mitano tangu Mbosso kuachana na WCB Wasafi, lebo iliyokuwa inamsimamia tangu 2018 na kumfanya kuwa mwanamuziki solo mkubwa.

Kabla ya hapo, Mbosso aliunda kundi la Yamoto Band na wenzake watatu (Aslay, Enock Bella na Beka Flavour) kati ya mwaka 2012 hadi 2017 walipotengana na kila mmoja kuanza kufanya muziki peke yake.

Chini ya WCB Wasafi yake Diamond Platnumz, mshindi wa MTV EMA's mara tatu, jina la Mbosso liligeuka kuwa chapa yenye ushawishi akishinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA), huku akitoa albamu, Definition of Love (2021) na EP, Khan (2022).

Room Number 3 EP (2025), ndio mradi wa kwanza chini ya Khan Music, lebo aliyoianzisha Mbosso kwa ajili ya muziki wake baada ya kusimamiwa na WCB Wasafi kwa miaka saba huku akiwa msanii wa sita kusainiwa.

Ndani ya mwezi mmoja pekee, EP hiyo imesıkılızwa zaıdı ya mara milioni 50 katika majukwaa yote ya muziki (digital streaming) ikiwa ni ya kwanza kwa Mbosso kufikia namba hizo ndani ya muda huo.

Kumbuka, namba hizo zimetoka katika majukwaa ya Spotify, Shazam, Deezer, Amazon Music, Tidal, iTunes, Boomplay, Audiomack, Google Play, SoundCloud na TikTok.

Hata hivyo, wimbo 'Pawa' umechangia karibia nusu ya namba hizo ukiwa umesikilizwa zaidi ya mara milioni 20, hivyo ndio wimbo uliopata mapokezi mazuri zaidi (most streamed) katika EP hiyo ambayo kwa sehemu kubwa imeandaliwa na S2kizzy.

Tukija YouTube, video yake imeshatazamwa zaidi ya mara milioni 11 ikiwa ni wiki tatu tangu kuachiwa, na hii ni ya kwanza kutoka kwa Mbosso kufanya hivyo ndani ya muda mfupi huku ikiwa namba moja Tanzania na Kenya kwa wiki tatu mfululizo.

Mafanikio ya wimbo huo na nyingine katika EP hiyo, imepelekea Mbosso kuwa msanii namba moja YouTube Kenya kati ya Julai 4 hadi 10, akifuatiwa na Marioo, Harmonize, Diamond, Vybz Kartel, Jay Melody na Bien, mwanachama wa kundi la Sauti Sol.

Ikumbukwe Room Number 3 EP (2025) inaonyesha safari ya muziki ya Mbosso na ukuaji wake, ikiwakilishwa vipindi vitatu tofauti, yaani Yamoto Band, WCB Wasafi na Khan Music akiwa kama msanii anayejitegemea.

Kila kipindi kinaonyesha hatua tofauti na muhimu katika safari hiyo kuanzia kipindi cha utafutaji na ukuaji, hadi alipo sasa akiwa na mamilioni ya mashabiki na wasikilizaji wa muziki wake mtandaoni duniani kote.

Kwa mchanganyiko wa hisia, uandishi wa hadithi nzuri na sauti iliyokomaa, Room Number 3 EP (2025) inaakisi umbali aliotoka Mbosso kimuziki, na haya ni matokeo ya shauku na dhamira ya kweli katika kuzifikia ndoto zake.

Utakumbuka, kwa mara ya kwanza Mbosso alipata umaarufu akiwa Yamoto Band baada ya kuachia wimbo wao, Ya Moto (2013) uliotengenezwa Vibe Records na Shirko, na kuanzia hapo jina lake limekuwa likijizolea sifa lukuki katika Bongofleva.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags